| Chapter 12 |
1 | Kwa hiyo, ndugu zangu, maadam Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: jitoleeni nafsi zenu kwa Mungu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye kupendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu. |
2 | Msiige mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza fikira zenu. Hapo ndipo mtakapoweza kuyajua mapenzi ya Mungu, kutambua jambo lililo jema, linalompendeza na kamilifu. |
3 | Kutokana na neema aliyonijalia Mungu, nawaambieni ninyi nyote: msijione kuwa ni kitu zaidi kuliko mnavyopaswa kuwa. Fikira zenu na ziwe na kiasi kufuatana na kipimo cha imani Mungu aliyomgawia kila mmoja. |
4 | Mwili una viungo vingi, kila kimoja na kazi yake. |
5 | Hali kadhalika ingawa sisi ni wengi, tu mwili mmoja kwa kuungana na Kristo, na kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. |
6 | Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kufuatana na neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha unabii na akitumie kadiri ya imani yake. |
7 | Mwenye kipaji cha utumishi na atumikie. mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe. |
8 | Mwenye kipaji cha kuwafariji wengine na afanye hivyo. Mwenye kumgawia mwenzake alicho nacho na afanye hivyo kwa ukarimu. Msimamizi na asimamie kwa bidii; naye mwenye kutenda jambo la huruma na afanye hivyo kwa furaha. |
9 | Mapendo yenu na yawe bila unafiki wowote. Chukieni jambo lolote ovu, zingatieni jema. |
10 | Pendaneni kidugu; kila mmoja amfikirie mwenzake kwanza kwa heshima. |
11 | Msilegee katika bidii, muwe wachangamfu rohoni katika kumtumikia Bwana. |
12 | Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida na kusali daima. |
13 | Wasaidieni watu wa Mungu katika mahitaji yao; wapokeeni wageni kwa ukarimu. |
14 | Watakieni baraka wote wanaowadhulumu ninyi; naam, watakieni baraka na wala msiwalaani. |
15 | Furahini pamoja na wanaofurahi, lieni pamoja na wanaolia. |
16 | Muwe na wema uleule kwa kila mtu. Msijitakie makuu, bali jishugulisheni na watu wadogo. Msijione kuwa wenye hekima sana. |
17 | Msilipe ovu kwa ovu. Zingatieni mambo mema mbele ya wote. |
18 | Kadiri inavyowezekana kwa upande wenu, muwe na amani na watu wote. |
19 | Wapenzi wangu, msilipize kisasi, bali mwachieni Mungu jambo hilo; maana Maandiko Matakatifu yasema: "Kulipiza kisasi ni shauri langu; mimi nitalipiza asema Bwana." |
20 | Tena, Maandiko yasema: "Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe kinywaji. Maana kwa kufanya hivyo utamfanya apate aibu kali kama makaa ya moto juu ya kichwa chake." |
21 | Usikubali kushindwa na ubaya, bali ushinde ubaya kwa wema. |