| Chapter 2 |
1 | Basi nimeamua nisiwatembelee tena kuwatia huzuni. |
2 | Maana nikiwahuzunisha ninyi, basi, ni nani atakayenifariji? Ni walewale niliowahuzunisha! |
3 | Ndiyo maana niliwaandikia--sikutaka kuja kwenu na kuhuzunishwa na ninyi ambao ndio mngepaswa kuwa furaha yangu. Nina hakika kwamba, mimi nikifurahi, ninyi nyote pia mnafurahi. |
4 | Nilipowaandikia hapo awali katika hali ya huzuni na sikitiko moyoni na kwa machozi mengi, haikuwa kwa ajili ya kuwahuzunisha ninyi, bali kwa ajili ya kuwaonyesheni kwamba nawapenda mno. |
5 | Ikiwa kuna mtu aliyemhuzunisha mwingine, hakunihuzunisha mimi--ila amewahuzunisha ninyi nyote, na sipendi kuwa mkali zaidi. |
6 | Adhabu aliyokwisha pata kutoka kwa wengi wenu inamtosha. |
7 | Iliyobakia ni afadhali kwenu kumsamehe mtu huyo na kumpa moyo ili asije akahuzunika mno na kukata tamaa kabisa. |
8 | Kwa hiyo nawasihi: mwonyesheni kwamba mnampenda. |
9 | Madhumuni yangu kuandika ile barua yalikuwa kutaka kujua kama mko tayari kutii katika kila jambo. |
10 | Mkimsamehe mtu, nami pia ninamsamehe. Maana ninaposamehe--kama kweli ninacho cha kusamehe--nasamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu, |
11 | ili tusimpe nafasi Shetani atudanganye; maana twaijua mipango yake ilivyo. |
12 | Nilipofika Troa kuhubiri Habari Njema ya Kristo, nilikuta mlango u wazi kwa ajili ya kazi ya Bwana. |
13 | Lakini nilifadhaika sana kwa kutomkuta ndugu yetu Tito. Ndiyo maana niliwaaga wote pale nikaenda Makedonia. |
14 | Lakini, shukrani kwa Mungu anayetuongoza daima katika msafara wa ushindi wa Kristo. Yeye hutufanya tuueneze ukweli wa Kristo kama harufu nzuri, kila mahali. |
15 | Maana sisi ni kama harufu nzuri ya ubani ambayo Kristo anamtolea Mungu, harufu nzuri inayofikia wote wanaookolewa na wanaopotea. |
16 | Kwa wale wanaopotea, harufu hiyo ni kifo; lakini kwa wale wanaookolewa, harufu hiyo ni uhai. Nani basi, awezaye kushiriki katika kazi ya namna hiyo? |
17 | Sisi si kama wengine ambao hufanya biashara na ujumbe wa Mungu; sisi tunahubiri kwa unyofu mbele ya Mungu, kama watu tuliotumwa na Mungu, tukiwa tumeungana na Kristo. |