| Chapter 4 |
1 | Nanyi wakuu, watendeeni watumwa wenu kwa uadilifu na haki, mkikumbuka kwamba nanyi pia mnaye Bwana mbinguni. |
2 | Dumuni katika sala, na mnaposali muwe waangalifu, mkimshukuru Mungu. |
3 | Vilevile, mtuombee sisi pia ili Mungu atupe fursa ya kuuhubiri ujumbe wake kuhusu siri ya Kristo. Kwa ajili hiyo mimi niko sasa kifungoni. |
4 | Basi, ombeni ili niweze kusema kama inavyonipasa na kwa namna itakayodhihirisha siri hiyo. |
5 | Muwe na hekima katika uhusiano wenu na watu wasioamini, mkitumia vizuri kila nafasi mliyo nayo. |
6 | Mazungumzo yenu yanapaswa kuwa daima mema na ya kuvutia, na mnapaswa kujua jinsi ya kumjibu vizuri kila mmoja. |
7 | Ndugu yetu mpenzi Tukiko, mfanyakazi mwaminifu na mtumishi mwenzetu katika kazi ya Bwana, atawapeni habari zangu zote. |
8 | Ndiyo maana namtuma, ili aichangamshe mioyo yenu kwa kuwaambieni habari zetu. |
9 | Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpenzi na mwaminifu, ambaye ni mwananchi mwenzenu. Watawapeni habari za mambo yote yanayofanyika hapa. |
10 | Aristarko, ambaye yuko kifungoni pamoja nami, anawasalimuni; hali kadhalika Marko, binamu yake Barnaba, (mmekwisha pata maagizo juu yake; akifika kwenu mkaribisheni). |
11 | Naye Yoshua aitwaye Yusto, anawasalimuni. Miongoni mwa Wayahudi waliokwisha pokea imani, hawa tu peke yao, ndio wanaofanya kazi pamoja nami kwa ajili ya Utawala wa Mungu; nao wamekuwa msaada mkubwa kwangu. |
12 | Epafra, mwananchi mwenzenu na mtumishi wa Kristo Yesu anawasalimuni. Daima anawaombeeni ninyi kwa bidii ili mpate kusimama imara, mkomae na kuwa thabiti kabisa katika mambo yote anayotaka Mungu. |
13 | Naweza kushuhudia kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu na kwa ajili ya watu wa Laodikea na Hierapoli. |
14 | Luka, daktari wetu mpenzi, na Dema, wanawasalimuni. |
15 | Salamu zetu kwa ndugu zetu wa Laodikea; msalimuni dada Nimfa pamoja na jumuiya yote ya waumini inayokutana nyumbani kwake. |
16 | Mkisha soma barua hii, hakikisheni kwamba inasomwa na Wakristo wa Laodikea; na ninyi fanyeni mpango mpate kuisoma barua waliyoipata kwao. |
17 | Mwambieni Arkipo aitekeleze vizuri ile huduma aliyokabidhiwa na Bwana. |
18 | Naandika haya kwa mkono wangu mwenyewe: Salamu kutoka kwangu, mimi Paulo. Kumbukeni kwamba niko kifungoni. Neema ya Mungu iwe nanyi. |