| Chapter 7 |
1 | "Msiwahukumu wengine, msije nanyi mkahukumiwa na Mungu; |
2 | kwa maana jinsi mnavyowahukumu wengine, ndivyo nanyi mtakavyohukumiwa; na kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho Mungu atakachotumia kwenu. |
3 | Kwa nini wakiona kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako? |
4 | Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, `Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako`, wakati wewe mwenyewe unayo boriti jichoni mwako? |
5 | Mnafiki wewe! Ondoa kwanza boriti iliyoko jichoni mwako na hapo ndipo utaona waziwazi kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilichoko jichoni mwa ndugu yako. |
6 | "Msiwape mbwa vitu vitakatifu wasije wakageuka na kuwararua ninyi; wala msiwatupie nguruwe lulu zenu wasije wakazikanyaga. |
7 | "Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata; bisheni, nanyi mtafunguliwa. |
8 | Maana, aombaye hupewa, atafutaye hupata, na abishaye hufunguliwa. |
9 | Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba mkate, atampa jiwe? |
10 | Au je, akimwomba samaki, atampa nyoka? |
11 | Kama basi ninyi, ingawa ni waovu, mwajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika Baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi: atawapa mema wale wanaomwomba. |
12 | "Watendeeni wengine yale mnayotaka wao wawatendee ninyi. Hii ndiyo maana ya Sheria ya Mose na mafundisho ya manabii. |
13 | "Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba. Kwa maana njia inayoongoza kwenye maangamizi ni pana, na mlango wa kuingilia humo ni mpana; waendao njia hiyo ni wengi. |
14 | Lakini njia inayoongoza kwenye uzima ni nyembamba, na mlango wa kuingilia humo ni mwembamba; ni watu wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo. |
15 | "Jihadharini na manabii wa uongo. Wao huja kwenu wakionekana kama kondoo kwa nje, lakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali. |
16 | Mtawatambua kwa matendo yao. Je, watu huchuma zabibu katika miti ya miiba, au tini katika mbigili? La! |
17 | Basi, mti mwema huzaa matunda mema, na mti mbaya huzaa matunda mabaya. |
18 | Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mema. |
19 | Kila mti usiozaa matunda mema utakatwa na kutupwa motoni. |
20 | Kwa hiyo, mtawatambua kwa matendo yao. ic |
21 | "Si kila aniambiaye, `Bwana, Bwana,` ataingia katika Ufalme wa mbinguni; ila ni yule tu anayetimiza mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. |
22 | Wengi wataniambia Siku ile ya hukumu: `Bwana, Bwana! kwa jina lako tulitangaza ujumbe wako, na kwa jina lako tuliwatoa pepo na kufanya miujiza mingi.` |
23 | Hapo nitawaambia: `Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni mbele yangu, enyi watenda maovu.` |
24 | "Kwa sababu hiyo, kila mtu anayeyasikia maneno yangu na kuyazingatia, anafanana na mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba. |
25 | Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo. Lakini haikuanguka kwa sababu ilikuwa imejengwa juu ya mwamba. |
26 | "Lakini yeyote anayesikia maneno yangu haya bila kuyazingatia, anafanana na mtu mpumbavu aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga. |
27 | Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo, nayo ikaanguka; tena kwa kishindo kikubwa." |
28 | Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, umati wa watu ukashangazwa na mafundisho yake. |
29 | Hakuwa kama walimu wao wa Sheria, bali alifundisha kwa mamlaka. |