| Chapter 10 |
1 | Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa uwezo wa kutoa pepo wachafu na kuponya magonjwa na maradhi yote. |
2 | Majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya: wa kwanza ni Simoni aitwae Petro, na Andrea ndugu yake; Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohane ndugu yake; |
3 | Filipo na Bartholomayo, Thoma na Mathayo aliyekuwa mtoza ushuru; Yakobo mwana wa Alfayo, na Thadayo; |
4 | Simoni Mkanaani, na Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu. |
5 | Yesu aliwatuma hao kumi na wawili na kuwapa maagizo haya: "Msiende kwa watu wa mataifa mengine, wala msiingie katika mji wa Wasamaria. |
6 | Ila nendeni kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo. |
7 | Mnapokwenda hubirini hivi: `Ufalme wa mbinguni umekaribia.` |
8 | Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo. Mmepewa bure, toeni bure. |
9 | Msichukue mifukoni mwenu dhahabu, wala fedha, wala sarafu za shaba. |
10 | Msichukue mkoba wa kuombea njiani, wala koti la ziada, wala viatu, wala fimbo. Maana mfanyakazi anastahili riziki yake. |
11 | "Mkiingia katika mji wowote au kijiji, tafuteni humo mtu yeyote aliye tayari kuwakaribisheni, na kaeni naye mpaka mtakapoondoka mahali hapo. |
12 | Mnapoingia nyumbani wasalimuni wenyeji wake. |
13 | Kama wenyeji wa nyumba hiyo wakiipokea salamu hiyo, basi, amani yenu itakaa pamoja nao. Lakini ikiwa hawaipokei, basi amani yenu itawarudia ninyi. |
14 | Kama mtu yeyote atakataa kuwakaribisheni au kuwasikilizeni, basi mtokapo katika nyumba hiyo au mji huo, yakung`uteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao. |
15 | Kweli nawaambieni, Siku ya hukumu mji huo utapata adhabu kubwa kuliko ile iliyoipata miji ya Sodoma na Gomora. |
16 | "Sasa, mimi nawatuma ninyi kama kondoo kati ya mbwa mwitu. Muwe na busara kama nyoka, na wapole kama njiwa. |
17 | Jihadharini na watu, maana watawapeleka ninyi mahakamani na kuwapiga viboko katika masunagogi yao. |
18 | Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu, mpate kutangaza Habari Njema kwao na kwa mataifa. |
19 | Basi, watakapowapeleka ninyi mahakamani, msiwe na wasiwasi mtasema nini au namna gani; wakati utakapofika, mtapewa la kusema. |
20 | Maana si ninyi mtakaosema, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. |
21 | "Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe, na baba atamsaliti mwanawe, nao watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua. |
22 | Watu wote watawachukieni kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ataokolewa. |
23 | "Watu wakiwadhulumu katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Kweli nawaambieni, hamtamaliza ziara yenu katika miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Mtu hajafika. |
24 | "Mwanafunzi si mkuu kuliko mwalimu wake, wala mtumishi si mkuu kuliko bwana wake. |
25 | Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mkubwa wa jamaa Beelzebuli, je hawatawaita watu wengine wa jamaa hiyo majina mabaya zaidi? |
26 | "Basi, msiwaogope watu hao. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, na kila kilichofichwa kitafichuliwa. |
27 | Ninalowaambieni ninyi katika giza, lisemeni katika mwanga; na jambo mlilosikia likinong`onezwa, litangazeni hadharani. |
28 | Msiwaogope wale wauao mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili pamoja na roho katika moto wa Jehanamu. |
29 | Shomoro wawili huuzwa kwa senti tano. Lakini hata mmoja wao haanguki chini bila kibali cha Baba yenu. |
30 | Lakini kwa upande wenu, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. |
31 | Kwa hiyo msiogope; ninyi mu wa thamani kuliko shomoro wengi. ic |
32 | "Kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, mimi pia nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. |
33 | Lakini yeyote atakayenikana hadharani, nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. |
34 | "Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga. |
35 | Maana nimekuja kuleta mafarakano kati ya mtu na baba yake, kati ya binti na mama yake, kati ya mkwe na mkwe wake. |
36 | Na maadui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake. |
37 | "Ampendaye baba au mama yake kuliko anipendavyo mimi, hanistahili. Ampendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. |
38 | Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata, hanistahili. |
39 | Anayeyashikilia maisha yake, atayapoteza; lakini anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata. |
40 | "Anayewakaribisha ninyi, ananikaribisha mimi; na anayenikaribisha mimi, anamkaribisha yule aliyenituma. |
41 | Anayemkaribisha nabii kwa sababu ni nabii, atapokea tuzo la nabii. Anayemkaribisha mtu mwema kwa sababu ni mtu mwema, atapokea tuzo la mtu mwema. |
42 | Kweli nawaambieni, yeyote atakayempa mmojawapo wa wadogo hawa kikombe cha maji baridi kwa sababu ni mfuasi wangu, hatakosa kamwe kupata tuzo lake." |