| Chapter 5 |
1 | Ndugu, hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya nyakati na majira yatakapotukia mambo haya. |
2 | Maana ninyi wenyewe mwajua kwamba Siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajavyo usiku. |
3 | Watu watakapokuwa wanasema: "Kila kitu ni shwari na salama" ndipo uharibifu utakapowaangukia ghafla! Mambo hayo yatatukia ghafla kama uchungu wa uzazi unavyomjia mama anayejifungua, wala watu hawataweza kuepukana nayo. |
4 | Lakini ninyi ndugu, hamko gizani, na siku hiyo haipaswi kuwajieni ghafla kama vile mwizi. |
5 | Ninyi nyote ni watu mnaoishi katika mwanga, watu wa mchana. Sisi si watu wa usiku, wala wa giza. |
6 | Basi, tusilale usingizi kama wengine; tunapaswa kukesha na kuwa na kiasi. |
7 | Wanaolala hulala usiku, na walevi hulewa usiku. |
8 | Lakini sisi ni watu wa mchana na tunapaswa kuwa na kiasi. Tunapaswa kuvaa imani na upendo kama vazi la kujikinga kifuani, na tumaini letu la wokovu kama kofia ya chuma. |
9 | Maana Mungu hakututeua ili tuangamizwe na ghadhabu yake, bali tuupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, |
10 | ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, iwe tu hai au tumekufa. |
11 | Kwa hiyo farijianeni na kusaidiana ninyi kwa ninyi kama mnavyofanya sasa. |
12 | Ndugu, tunawaombeni muwastahi wale wanaofanya kazi kati yenu, wale wanaowaongoza na kuwafundisheni kuhusu maisha ya Kikristo. |
13 | Wapeni heshima kubwa na kuwapenda kwa sababu ya kazi wanayofanya. Muwe na amani kati yenu. |
14 | Ndugu, tunawahimizeni muwaonye watu walio wavivu, muwatie moyo watu wanyonge, muwasaidie watu dhaifu, muwe na subira kwa wote. |
15 | Angalieni mtu yeyote asimlipe mwingine maovu kwa maovu, ila nia yenu iwe kutendeana mema daima na kuwatendea mema watu wote. |
16 | Furahini daima, |
17 | salini kila wakati |
18 | na muwe na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu. |
19 | Msimpinge Roho Mtakatifu; |
20 | msidharau unabii. |
21 | Pimeni kila kitu: zingatieni kilicho chema, |
22 | na epukeni kila aina ya uovu. |
23 | Mungu anayetupatia amani awafanye ninyi watakatifu kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu--roho, mioyo na miili yenu--mbali na hatia yoyote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. |
24 | Yeye anayewaita ninyi atafanya hivyo kwani ni mwaminifu. |
25 | Ndugu, tuombeeni na sisi pia. |
26 | Wasalimuni ndugu wote kwa ishara ya upendo. |
27 | Nawahimizeni kwa jina la Bwana muwasomee ndugu zetu wote barua hii. |
28 | Tunawatakieni neema ya Bwana wetu Yesu Kristo. |