| Chapter 3 |
1 | Ndugu zangu watu wa Mungu ambao mmeitwa na Mungu, fikirini juu ya Yesu ambaye Mungu alimtuma awe Kuhani Mkuu wa imani tunayoiungama. |
2 | Yeye alikuwa mwaminifu kwa Mungu aliyemteua kufanya kazi yake kama vile Mose alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu. |
3 | Mjenzi wa nyumba hupata heshima zaidi kuliko hiyo nyumba yenyewe. Hali kadhalika naye Yesu anastahili heshima kubwa zaidi kuliko Mose. |
4 | Kila nyumba hujengwa na mjenzi fulani--na Mungu ndiye mjenzi wa vitu vyote. |
5 | Mose alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Bwana kama mtumishi, na alinena juu ya mambo ambayo Mungu atayasema hapo baadaye. |
6 | Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana mwenye mamlaka juu ya nyumba ya Mungu. Sisi ni nyumba yake kama tukizingatia uhodari wetu na uthabiti wetu katika kile tunachotumainia. |
7 | Kwa hiyo, basi, kama asemavyo Roho Mtakatifu: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, |
8 | msiifanye mioyo yenu kuwa migumu kama wazee wenu walivyokuwa wakati walipomwasi Mungu; kama walivyokuwa siku ile kule jangwani, |
9 | Huko wazee wenu walinijaribu na kunichunguza, asema Bwana, ingawa walikuwa wameyaona matendo yangu kwa miaka arobaini. |
10 | Kwa sababu hiyo niliwakasirikia watu hao nikasema, `Fikira za watu hawa zimepotoka, hawajapata kamwe kuzijua njia zangu.` |
11 | Basi, nilikasirika, nikaapa: `Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko."` |
12 | Basi ndugu, jihadharini asije akawako yeyote miongoni mwenu aliye na moyo mbaya hivyo na asiyeamini hata kujitenga na Mungu aliye hai. |
13 | Maadamu hiyo "Leo" inayosemwa katika Maandiko bado inatuhusu sisi, mnapaswa kusaidiana daima, ili mtu yeyote miongoni mwenu asidanganywe na dhambi na kuwa mkaidi. |
14 | Maana sisi tunashirikiana na Kristo ikiwa tutazingatia kwa uthabiti tumaini tulilokuwa nalo mwanzoni. |
15 | Maandiko yasema hivi: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, msiifanye mioyo yenu kuwa migumu kama wazee wenu walivyokuwa wakati walipomwasi Mungu." |
16 | Ni akina nani basi, waliosikia sauti ya Mungu wakamwasi? Ni wale wote walioongozwa na Mose kutoka Misri. |
17 | Mungu aliwakasirikia akina nani kwa miaka arobaini? Aliwakasirikia wale waliotenda dhambi, maiti zao zikatapakaa kule jangwani. |
18 | Mungu alipoapa: "Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko," alikuwa anawasema akina nani? Alikuwa anasema juu ya hao walioasi. |
19 | Basi, twaona kwamba hawakuingia huko kwa sababu hawakuamini. |