Swahili New Testament Bible

Matthew

Return to Index

Chapter 1

1

Yesu Kristo alikuwa mzawa wa Daudi, mzawa wa Abrahamu. Hii ndiyo orodha ya ukoo wake:

2

Abrahamu alimzaa Isaka, Isaka alimzaa Yakobo, Yakobo alimzaa Yuda na ndugu zake,

3

Yuda alimzaa Faresi na Zera (mama yao alikuwa Tamari), Faresi alimzaa Hesroni, Hesroni alimzaa Rami,

4

Rami alimzaa Aminadabu, Aminadabu alimzaa Nashoni, Nashoni alimzaa Salmoni,

5

Salmoni alimzaa Boazi (mama yake Boazi alikuwa Rahabu). Boazi na Ruthi walikuwa wazazi wa Obedi, Obedi alimzaa Yese,

6

naye Yese alimzaa Mfalme Daudi. Daudi alimzaa Solomoni (mama yake Solomoni alikuwa mke wa Uria).

7

Solomoni alimzaa Rehoboamu, Rehoboamu alimzaa Abiya, Abiya alimzaa Asa,

8

Asa alimzaa Yehoshafati, Yehoshafati alimzaa Yoramu, Yoramu alimzaa Uzia,

9

Uzia alimzaa Yothamu, Yothamu alimzaa Ahazi, Ahazi alimzaa Hezekia,

10

Hezekia alimzaa Manase, Manase alimzaa Amoni, Amoni alimzaa Yosia,

11

Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake. Huo ulikuwa wakati Wayahudi walipopelekwa uhamishoni Babuloni.

12

Baada ya Wayahudi kupelekwa uhamishomi Babuloni: Yekonia alimzaa Shealtieli, Shealtieli alimzaa Zerobabeli,

13

Zerobabeli alimzaa Abiudi, Abiudi alimzaa Eliakimu, Eliakimu alimzaa Azori,

14

Azori alimzaa Zadoki, Zadoki alimzaa Akimu, Akimu alimzaa Eliudi,

15

Eliudi alimzaa Eleazeri, Eleazeri alimzaa Mathani, Mathani alimzaa Yakobo,

16

Yakobo alimzaa Yosefu, aliyekuwa mume wake Maria, mama yake Yesu, aitwaye Kristo.

17

Basi, kulikuwa na vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi mpaka Wayahudi walipochukuliwa mateka Babuloni, na vizazi kumi na vinne tangu kuchukuliwa mateka mpaka wakati wa Kristo.

18

Basi, hivi ndivyo Yesu Kristo alivyozaliwa: Maria, mama yake, alikuwa ameposwa na Yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

19

Yosefu, mumewe, kwa vile alikuwa mwadilifu, hakutaka kumwaibisha hadharani; hivyo alikusudia kumwacha kwa siri.

20

Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akamwambia, "Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, maana amekuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

21

Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye atawaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao."

22

Basi, haya yote yalitukia ili litimie lile neno Bwana alilosema kwa njia ya nabii:

23

"Bikira atachukua mimba, atamzaa mtoto wa kiume, naye ataitwa Emanueli" (maana yake, "Mungu yu pamoja nasi").

24

Hivyo, Yosefu alipoamka usingizini alifanya kama malaika huyo alivyomwambia, akamchukua mke wake nyumbani.

25

Lakini hakumjua kamwe kimwili hata Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu akampa jina Yesu.

Matthew 2

 

 

 

HTMLBible Software - Public Domain Software by johnhurt.com

 


Other Software is Available At These Sites: